
Na:
Albert Sanga, Iringa.
Kumekuwa na changamoto kubwa kwa
waliojiajiri na walioajiriwa kuhusu dhana ya mikopo na madeni. Licha ya
kwamba wakati mmoja hadi mwingine, wengi wetu tumepata kuwa na mikopo au
madeni; ni wachache wanaotambua maana halisi ya mikopo na madeni na
namna mambo haya mawili yanavyotakiwa kwenda nayo katika maisha ya
kiuchumi.
Tuchukulie mfano wa wafanyakazi. Wafanyakazi wengi huwa
wanajikuta wakiishiwa mishahara yao kabla hata ya tarehe ya kupokea
mshahara mwingine. Wakishamaliza mishahara yao huwa wanajikuta hawana
namna ya kumudu bejeti zao, ikiwemo chakula na usafiri; hivyo wanapata
mbinyo wa kuazima fedha, huduma au bidhaa kutoka kwa wenzao, katika
maduka na kutoka kwa watu binafsi.
Wakishaazima hizo fedha,
huduma au bidhaa; mioyo yao inasuuzika, wanamalizia siku zilizobaki
kabla ya mshahara. Mshahara unapotoka wanajikuta wanatakiwa kulipa
madeni yao, hivyo wengi wao huwa wanaanza kulipa yale madeni kisha
inayobaki ndio wanaanza kutumia matumizi mengine. Mtindo unakuwa ni ule
ule wa kuishiwa kabla ya mwisho wa mwezi. Kwa kadri mfanyakazi huyu
anavyoendelea kukopa madeni kwa mtindo wa namna hii; anaendelea
kuzalisha mfumo wa utegemezi unaokua. Ukifuatilia utabaini kuwa kama
mwezi huu mshahara ulikuwa unaisha tarehe 20, basi mwezi ujao utaisha
tarehe 15, na unaofuata utakuwa unaisha tarehe 10!Mwisho wa siku
mshahara wa mfanyakazi huyu usishangae kuona unaisha tarehe 2 ya mwezi!
Kwa nini wafanyakazi na watu wengine waendelee kuishi maisha ya aina hii
wakati fedha inapita mikononi mwao? Natambua wengi watasema tatizo ni
kuwa mishahara wanayolipwa haitoshi, lakini ukweli ni kwamba tatizo
kubwa ni kwamba, wengi hawaelewi namna ya kutumia fedha na jinsi ya
kumudu madeni na mikopo.
Kanuni inasema kwamba kila fedha
inayopita mkononi mwako unatakiwa kuichukulia kama mbegu. Ikipita
shilingi kumi ni lazima itoke mikononi mwako ikiwa zaidi ya shilingi
kumi. Hapo ndipo ilipo akili ya matumizi ya fedha. Kwa namna maisha
yalivyo na halihalisi ya mishahara mingi ilivyo ni vigumu kukwepa suala
la kukopa (na hata madeni).
Kwa ujumla hakuna ubaya wa kukopa,
lakini kuna tofauti kati ya mkopo na deni. Mkopo ni fedha ama mali
inayoazimwa kutoka kwa mtu ama kutoka kwa taasisi; kwa makubaliano ya
kurejeshwa katika kipindi fulani; kwa madhumuni ya matumizi ya kuzalisha
fedha zaidi ama mali zaidi. Wakati deni ni a) Fedha ama mali
iliyoazimwa kwa ajili ya matumizi yasiyozalisha fedha ama mali zaidi b)
deni ni mkopo uliopita muda wa makubaliano ya kulipwa.
Ndio maana
mtu akienda kukopa fedha benki (kwa madhumuni ya kufanyia biashara)
utasikia yule bwana ana mkopo, lakini akishindwa kurejesha mkopo ule kwa
wakati uliopo kwenye makubaliano; utasikia yule bwana ana deni! Bahati
mbaya ni kwamba kuna watu wengi sana ambao huwa wanachanganya kati ya
deni na mkopo.
Wengi wana madeni lakini utasikia wanasema wana
mikopo. Mtu anachukua fedha benki kwa dhamana ya mshahara wake kisha
fedha hiyo anakwenda kununulia seti ya runinga, sofa na kununulia
viwalo, halafu anajifariji kuwa ana mkopo, la hasha! Hilo ni deni.
Wengine huchukua fedha benki na kununulia magari ya kutembelea nao
hujifariji kwamba wana mikopo; sio kweli hawa ni kwamba wana madeni.
Tena hawa wenye kuchukua fedha na kununulia magari ya kutembelea ambayo
hayawaingizii chochote zaidi ya kuwalamba fedha zao; wanatakiwa kuyaita
“madeni ya kutembelea” na sio magari ya kutembelea.
Katika nukta
hii, namna nzuri ya kutumia fedha ni pamoja na kutambua vema nafasi ya
mkopo na deni kwako. Unaamini nini kuhusu mikopo na madeni? Una uthubutu
na tabia gani linapokuja suala la kudaiwa? Unahimili vipi madeni yako?
Haya ni mambo ya kuyajua na kuyarekebisha yakae katika uelekeo sahihi
kwa sababu yanaamua sana namna unavyoweza kutumia fedha zako.
Kukopa
ni suala zuri sana. Biashara zote duniani zilianzishwa, haunzishwa na
zitaendelea kuanzishwa kwa kutumia mikopo. Iwe umechukua hela mfukoni
mwako na kuanzisha biashara huo ni mkopo, iwe umepewa fedha, huo ni
mkopo kwa biashara yako.
Hata kama mkopo huo hauna riba wala
hauhitaji kurudishwa hilo haliondoi uhalisia wa kwamba ni mkopo na
katika mizania ya kihasibu mtaji wa kila biashara unatakiwa kuonesha
kuwa mtaji wa mwanzo ni mkopo. Hata watu binafsi, iwe ni walioajiriwa
ama laa, wenye cha kufanya ama wasio na cha kufanya; ukweli ni kwamba
kuna wakati kwenye maisha utapungukiwa na utahitaji kukopa.
Unaweza
kukopa benki, kwenye taasisi nyingine ama kwa mtu binafsi, kote huko ni
kukopa. Imani yako kuhusu mikopo itaamua sana namna unavyotumia fedha
zako katika kulipa ama kutokulipa. Bahati mbaya ni kwamba tunao
watanzania wengi ambao hawataki hata kidogo kusikia habari za mikopo.
Hawa utawasikia wakisema, “Mikopo haina maana”, “Kukopa ni umasikini”,
“Ukitaka kufilisika jaribu kukopa”. Kama muhusika anaamini hivi uwe na
uhakika kwamba ufahamu wake utapeleka taarifa katika ubongo inayoonesha
kwamba mkopo ni utumwa!
Sheria ya uvutano wa kimaumbile (Law of
attraction) inasema kwamba chochote anachokiogopa mtu hutokea na
chochote anachokiogopa mtu hukiabudu na chochote mtu anachokiabudu
hudhihirika. Mtu anaeamini kuwa mikopo haifai ikitokea amekopa
atakachojitahidi ni kuhakikisha kuwa anahangaika kuulipa mkopo huo ama
deni hilo haraka haraka.
Ikiwa mtu huyu ni mfanyakazi ndio
atarudi kule mwanzo ambapo kila akipata mshahara atakuwa anakimbilia
kurejesha deni analodaiwa. Kinachotokea? Ni kwamba ataendelea kukopa
tena na tena na kuendelea kuwa katika utumwa wa madeni na mwisho wa siku
akishalemewa atajidhihirishia yeye mwenyewe imani yake ya kwamba kukopa
ni utuwa na mateso.
Bahati mbaya wapo wazazi ambao huwaaminisha
watoto wao tangu wakingali wadogo ama wakiwa makazini ya kwamba mikopo
ni mibaya. Hata wale wanaokopa kupitia makato ya mishahara yao hawawi
salama ikiwa wana imani mfu kuhusu mikopo na madeni. Kwa sababu
aliyechukua mkopo na kwenda kununua gari ama kununua fenicha za ndani,
siku mshahara unapoanza kukatwa na kujikuta haumtoshelezi atageuka na
kuanza kunung’unikia madeni kwa ukali wa makato anayoyapata.
Nini
maana yake mambo hayo ya madeni na mikopo? Kumbuka kwamba tunaangalia
namna ya kuwa na matumizi mazuri ya fedha. Na nimesema kwamba matumizi
mzuri ya fedha ni kutumia fedha katika mtiririko unaokuimarishia uchumi
wako na sio kukudidimza.
Sasa, kuna wakati katika maisha unaweza
kupitia katika changamoto ya madeni. Huenda ulichukua fedha eidha kwa
mtu ama katika taasisi kwa lengo zuri la kuzalisha, lakini mambo
yakaenda mrama na ukajikuta mkopo umegeuka kuwa deni na huna namna ya
kulipa kwa wakati husika. Lakini pia huenda ulichukua fedha na
kuielekeza katika matumizi ya ‘kimadeni-madeni’ na unatakiwa kulipa.
Walisema waswahili ya kwamba dawa ya deni ni kulipa; hilo ni kweli
lakini unatakiwa kulipa deni lako na wakati huo huo uchumi wako
uimarike.
Kama ulichukua mkopo benki kwa dhamana ya mali zako;
hilo nitalileta kwa kina zaidi katika makala yenye kichwa,
“Wajasiriamali na jinamizi la mikopo”. Lakini kote kote, iwe ni kutoka
benki, iwe umekopa kwa mtu ama iwe umekopa dukani (na ukajikuta una
deni) ni lazima sana uhakikishe unalipa kwa akili.
Kuchukua
mshahara wote na kulipa madeni hakutakusaidia zaidi ya kukuangamiza.
Kuchukua faida yote na kuipeleka kwa wadeni nako kutakuachia umasikini.
Ukiwa katika hali hii ni lazima uzikumbuke tabia za kitajiri;
kuhakikisha unatenga kwanza akiba kisha mengine yanafuatia.
Hata
kama kuna mbinyo mkali kiasi gani ili ujikwamue na madeni ni lazima
uhakikishe unatenga sehemu ya mshahara ama faida yako kwa ajili ya akiba
(nap engine uwekezaji) na inayobaki ndipo iende kwa kulipa madeni na
matumizi ya kawaida (yale matumizi yasiyozalisha). Kujua namna nzuri ya
kutumia fedha ni pamoja na kuwa imara na mwenye msimamo dhidi ya
wanaokudai.
Wanaokudai wanaweza kuwa na vishondo vikubwa kweli
kweli, wanaweza kuwa na matisho makali kweli kweli, lakini muda wote
jitahidi kuvumilia vishondo na matisho yao na kamwe matisho na vishindo
vyao visikutoe kwenye kanuni hii, “Madeni yote yalipwe baada ya kutenga
akiba”.
Kwa wale waamini wanaozingatia masuala ya sadaka, kanuni hii
inanyumbuka na kuwa “Madeni yote yalipwe baada ya kutenga sadaka na
akiba”. Madeni ni changamoto na ni kitu ambacho kinatakiwa kuchukuliwa
kama kipindi cha mpito kwa mtu yeyote anaepambana kuimarisha uchumi
wake.
Kwenye kitabu cha The Richest Man In Babylon; tunapewa maarifa
kwamba haijalishi upo kwenye madeni makubwa na magumu kiasi gani, njia
rahisi ya kujikomboa kiuchumi ni kuhakikisha unatenga si chini ya
asilimia kumi ya kila fedha unayoipata; na kisha kuanza kuitumia ile
fedha uliyotenga kwa ajili ya kuwekeza na kuzalisha.
Sote tunastahili ushindi wa kifedha na kiuchumi.
#PoweredBySisiVijanaTanzania